Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga leo Jumamosi saa kumi jioni wanashuka katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya kuikabili Mbeya City katika mchezo wa ligi kuu raundi ya 18.
Yanga iko mkoani Mbeya tangu juzi ikijifua tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.
Hii ni mara ya pili kwa Yanga kucheza katika dimba la Sokoine mwezi huu kwani Disemba 03 ilicheza na Tanzania Prisons na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo ambao ulitawaliwa na vurugu za hapa na pale kutokana na maamuzi yasiyorodhisha.
Mkongwe Amissi Tambwe ndiye aliyeibeba Yanga katika mchezo huo, ambapo alifunga mabao mawili huku akihusika kwenye bao la kusawazisha lililofungwa kwa mkwaju wa penati na Ibrahim Ajib
Tambwe yuko katika kiwango bora kabisa na hakuna shaka leo akiwa na Mcongoman kinara wa mabao Heritier Makambo, wataongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga.
Yanga itawakosa baadhi ya wachezaji wake ambao hawakusafiri na timu hiyo kutokana na majeruhi au dharura.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Papi Tshishimbi ambaye bado hajarejea nchini kutoka DR Congo alikokwenda kuhudhuria msiba wa mkwe wake.
Raphael Daudi, Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi na Andrew Vicent wao ni majeruhi wakati mlinda lango Beno Kakolanya anaendelea kukosekana akisubiri huruma ya kocha Mwinyi Zahera.
Nae kocha Zahera amesema mchezo huo hautakuwa mwepesi lakini amewaandaa vijana wake kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili waendelee kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi.