Hakuna ubishi mshambuliaji Amissi Tambwe amerejea kwenye umahiri wake wa kupachika mabao leo akiiongoza Yanga kupata ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa raundi ya tatu kombe la FA dhidi ya Tukuyu Stars.

Tambwe ameondoka na mpira baada ya kutupia kambani mabao matatu 'hat-trik' huku bao la tatu akilifunga kwa kuubetua mpira juu ya mlinda lango New Afrika mfano wa mshambuliaji wa FC Barcelona Lionel Messi.
Huyu ndiye Tambwe ambaye WanaYanga wanamfahamu. Akiwa kwenye ubora wake hakuna mshambuliaji hapa nchini anayeweza kumfikia katika umahiri wa kupachika mabao.
Tofauti na washambuliaji wengi, Tambwe haihitaji nafasi nyingi sana kufunga. Ukimpatia nafasi mbili anao uwezo wa kukufungia bao moja.
Inafahamika msimu uliopita haukuwa mzuri kwake sababu ikiwa ni majeraha ya goti yaliyomuweka nje karibu msimu mzima.
Lakini msimu huu tayari amepachika mabao matano kwenye ligi na kasi yake ya kufunga haionekani kupungua.
Kurejea kwa Tambwe katika ubora wake ni habari njema kwa Yanga ambayo haikuongeza mshambuliaji wakati wa dirisha dogo la usajili kutokana na changamoto za kiuchumi.