MAPINDUZI makubwa ya teknolojia katika soka la vilabu barani Afrika yanatarajiwa kushuhudiwa kuanzia mwishoni mwa wiki hii, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupanua matumizi ya teknolojia ya usaidizi wa mwamuzi kwa njia ya video (VAR) hadi hatua ya makundi ya michuano yake ya vilabu.
Tofauti na misimu iliyopita, ambapo teknolojia hiyo imekuwa ikitumika kuanzia hatua ya robo fainali, msimu huu wa 2026/27 matumizi yake yanatarajiwa kuanza mapema zaidi.
Teknolojia hiyo itatumika katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), ambazo hatua zake za makundi zinaanza Novemba 27 hadi 29.
Hatua hiyo inalenga kuboresha kiwango cha uamuzi, kupunguza makosa ya waamuzi na kuimarisha haki katika mashindano hayo.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unakwenda vizuri, CAF ilichagua waamuzi 35 wa daraja la juu kwa ajili ya mafunzo maalumu yaliyofanyika kuanzia Novemba 18 hadi 23, jijini Cairo, Misri.
Aidha, waamuzi wengine 15 walichaguliwa kwa ajili ya mafunzo maalumu yanayohusu matumizi ya teknolojia ya VAR.
Kabla ya hapo, CAF iliandaa semina ya siku mbili kwa wawakilishi wa vilabu vilivyofuzu hatua ya makundi, ambapo masuala ya uamuzi na taratibu za matumizi ya VAR yalikuwa miongoni mwa mada zilizopangwa kujadiliwa.