Kiungo kiraka wa Yanga Maxi Nzengeli hajaonekana kwenye kikosi cha Wananchi kinachoendelea na maandalizi yake Zanzibar wakati huu ambao ligi imesimama kupisha kalenda ya FIFA.
Maxi amebaki jijini Dar es salaam akiendelea na matibabu ya jeraha la goti alilopata kwenye mchezo wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amethibitisha kuwa nyota huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameachwa Dar es Salaam chini ya uangalizi wa jopo la madaktari.
"Ni kweli, kiungo wetu Maxi Nzengeli amebaki Dar es Salaam kufuatia majeraha ya goti aliyoyapata kwenye mchezo wetu uliopita dhidi ya Kagera Sugar," alisema Kamwe. Kamwe
Kamwe aliongeza kuwa Maxi anaendelea kufanyiwa vipimo zaidi na matibabu, na wana matumaini makubwa kuwa mapumziko haya yatamsaidia kurejea uwanjani mapema ili kuwahi mchezo wa kwanza wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger unaotarajiwa kupigwa Novemba 28..
Wakati Maxi akiendelea kuimarika, habari njema kwa Wananchi ni urejeo wa kiungo Duke Abuya ambaye ameanza rasmi mazoezi ya timu visiwani Zanzibar.
Abuya anaweza kuwa tayari kuwakabili Polisi Tanzania kwenye mchezo wa ligi kuu utakaopigwa Novemba 20 uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro.