Jana mshambuliaji Ibrahima Toure aliwakumbusha daraja lake wale wanaombeza akifunga moja ya mabao ambayo yana sifa ya kuwania na tuzo ya goli bora la msimu.
Ni katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa uwanja wa KMC Complex Toure akiweka kambani mabao licha ya kucheza kwa takribani dakika 15 akiisaidia Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0
Licha ya kupata muda finyu wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza, Toure tayari amepachika mabao matatu kwenye ligi huku pia akiwa amefunga mabao mawili kwenye ligi ya mabingwa. Jumla amefunga mabao matano kwenye mashindano yote.
Toure ni mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa akicheza kwa muda mrefu Arabuni, uzoefu huo huenda ukawa msaada mkubwa kwa Yanga kuanzia hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa.
Tofauti na Peter Shalulile ambaye ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi cha Yanga kwenye ligi akiwa amefunga mabao 6, Toure amejipambanua kuwa mshambuliaji ambaye hahitaji nafasi nyingi kufunga.
Anafahamu kukaa kwenye maeneo sahihi, akiwapa wakati mgumu walinzi wa timu pinzani kumdhibiti kutokana na umbile na aina yake ya uchezaji. Lakini pia faida nyingine kubwa kwake ni uwezo wake wa kutumia miguu yote miwili.
Eneo la ushambuliaji unaweza kusema msimu huu Yanga imejitosheleza kwani urejeo wa Clement Mzize na uwepo wa Seleman Mwalimu umeongeza ushindani katika eneo hilo.