Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga watakuwa dimba la KMC Complex kuikaribisha Kagera Sugar.
Ni mchezo wa mzunguuko wa 10 utakaopigwa saa 1 usiku. Ni wazi Yanga itashuka kwenye mchezo huo ikiwa na dhamira moja tu, kusaka ushindi ili kurejea katika nafasi ya pili na kuendelea kuwapa presha watani zao Simba kwenye mbio za ubingwa.
Ligi inatarajiwa kusimama kwa takribani wiki tatu kupisha kalenda ya FIFA, matokeo tofauti na ushindi kwa Wananchi ni wazi yatawaweka mashabiki wa timu hiyo katika kipindi kigumu mbele ya watani zao ambao msimu huu 'wamejipata'
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Simon Dladla ameweka wazi dhamira ya kikosi chake ni kuibuka na ushindi huku akikiri haitakuwa mechi nyepesi.
Kagera Sugar inayonolewa na kocha Cedric Kaze, inapambana kujiondoa nafasi za chini kwenye msimamo hivyo ni wazi wanakwenda kuwapa Wananchi mechi ngumu.
Kaze ana historia na Yanga, akicheza dhidi ya timu ambayo ilimpa mafanikio makubwa zaidi kwenye historia yake ya ukocha.
Alipita Yanga katika nyakati mbili tofauti akiwa kocha mkuu na baadae kuwa kocha msaidizi wakati huo Yanga ikinolewa na Nasredinne Nabi.
Zitakuwa dakika 90 za moto pale uwanja wa KMC Complex.