Inaelezwa tayari uongozi wa Yanga umekamilisha mchakato wa kumpata kocha mpya na wakati wowote kocha huyo atatangazwa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema kocha mpya huenda akawa jukwaani pale KMC Complex siku ya Jumapili wakati Yanga itakapokuwa ikichuana na Kagera Sugar.
Kuna majina matatu makubwa ambayo yamehusishwa kurithi mikoba iliyoachwa na Manqoba Mngqithi.
Krunoslav Jurcic
Kocha raia wa Kroatia anaripotiwa kufanya mazungumzo na Yanga kupitia wasimamizi wake. Hata hivyo, inaelezwa changamoto kubwa ilikuwa upande wa mshahara aliotaka unaokadiriwa kufikia Dola 60,000 kwa mwezi (zaidi ya Shilingi milioni 160 za Kitanzania), kiasi ambacho ni mara tatu ya alichokuwa akipokea Manqoba.
Uongozi wa Yanga umeweka malengo makubwa ya kufanya vyema kwenye ligi ya mabingwa msimu huu droo ya makundi ikifanyika Misri jana na Yanga kupangwa kundi la kifo lenye timu ngumu Club Africain, MC Alger na Zamalek.
Jurcic ni kocha mzoefu ambaye tayari ameonja mafanikio ya makubwa ngazi ya klabu Afrika akiiongoza Pyramids kutwaa taji la ligi ya mabingwa kwa mara ya kwanza.
Fadlu Davids
Aliyekuwa kocha wa Simba SC, na klabu ya Raja Casablanca, nae anatajwa kuwa miongoni mwa makocha waliojadiliwa. Taarifa za ndani zinabainisha kuwa Fadlu alikaribia kutua Yanga kabla ya ujio wa Manqoba mpango wake ukikwama mwishoni kutokana na kutofikiwa kwa makubaliano upande wa maslahi.
Kocha huyo bado hana timu tangu alipoachana na klabu ya Raja CA ya Morocco ambayo aliiongoza kwa sehemu kubwa ya msimu uliopita lakini akaondolewa kwenye nafasi yake mwishoni baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Morocco.
Sead Ramovic
Pengine huyu ndio kocha ambaye mashabiki wa Yanga watatamani arejee tena Jangwani kutokana na kazi aliyoifanya katika muda mfupi aliowatumikia Wananchi 2024/25 kabla ya kunyakuliwa na CR Belouizdad waliolipa fedha nyingi kuvunja mkataba wake na Yanga.
Wengi wanaamini aina ya soka ambalo analifundisha Ramovic, 'Gusa Achia Twende Kwao' ndio soka ambalo linaweza kuipa Yanga mafanikio.
Ni wazi kama haitawezekana kumpata Jurcic ambaye aliiongoza Pyramids kutwaa Taji la Ligi ya Mabingwa 2024/25, Wananchi watatamani kuwa na Ramovic zaidi kuliko Fadlu.
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kwa hamu kubwa kumfahamu kocha wao mpya kwani hakuna tena muda wa kusubiri. Kocha huyo anapaswa kuanza majukumu yake mapema ili kukiimarisha kikosi kabla ya mikiki mikiki ya hatua ya makundi CAFCL kuanza mwishoni mwa mwezi ujao.