Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Simon Dladla amewahakikishia mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuwa kikosi chao kiko tayari kujisahihisha baada ya kutofanya vyema kwenye michezo miwili iliyopita ya ligi kuu.
Kesho Yanga itashuka uwanja wa KMC Complex kuikabili Mashujaa Fc katika mchezo mwingine ambao Wananchi wanahitaji matokeo ya aina moja tu, ushindi ili kusalia kwenye nafasi nzuri katika mbio za ubingwa.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Dladla alisema wanafahamu waliwaumiza mashabiki wao kwa kukosa matokeo mazuri kwenye mchezo uliopita. Dladla amesema wachezaji wanafahamu nini mashabiki wao wanahitaji na hivyo kesho watakuwa 'wakali' na watapambana ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
“Tunacheza nyumbani, hivyo ni lazima tuwe wakali na wenye maamuzi haraka na sahihi mbele ya lango. Tunapaswa kutumia vizuri nafasi zetu na kuhakikisha tunapata matokeo tunayoyahitaji. Sisi ni wataalamu wa mchezo huu na tunaelewa changamoto zinazotukabili. Ninaamini tuko tayari.“
“Mchezo uko mikononi mwa wachezaji. Wanajua nini cha kufanya. Mabadiliko ya kimfumo na kimbinu itategemea wachezaji watakaopatikana. Kama nilivyosema, tutakuwa wakali na tutacheza mchezo wa kuvutia. Tunajua changamoto zetu, tunazifanyia kazi. Malengo makubwa ya Yanga ni kuhakikisha tunakuwa namba moja.”
“Kwa Wananchi, tunafahamu kuwa tuliwakatisha tamaa katika mchezo uliopita kwa sababu hatukupata matokeo tuliyokuwa tunayatarajia. Tumeyatambua mapungufu yetu na tutafanya kazi kwa bidii. Tunafahamu kuwa tuna deni kubwa kwenu. Tunadaiwa magoli, tunadaiwa soka zuri na kiwango cha juu cha ushindani kila tunaposhuka uwanjani.”
“Rai yangu kwa mashabiki wa klabu hii tunaomba mtupe muda na muendelee kutuunga mkono. Kuweni na imani ma wachezaji na viongozi wenu. Njooni kwa wingi uwanjani kutusapoti. Tutahakikisha tunapambana ili kuwarudishia tabasamu na kuwapa furaha kupitia matokeo mazuri. Kila mmoja wetu anatambua matarajio ya mashabiki wetu na umuhimu wa kuonyesha mwitikio ndani ya uwanja,” alisema