Mashabiki wa Yanga wakiona picha hiyo juu ni wazi wanamkumbuka Adnan Behlulovic aliyekuwa kocha wa viungo wakati Yanga ikinolewa na kocha Sead Ramovic.
Ukweli ni kwamba katika nyakati bora kwenye misimu ya karibuni, Wananchi walifurahia soka ni wakati wa Ramovic na baadae akafuatia Miloud Hamdi ambaye bado jina lake halijatoka kweny midomo ya Wananchi.
Kwa sasa Yanga iko sokoni kusaka kocha mkuu na kocha wa viungo baada ya hapo jana kutangaza kuwafuta kazi Manqoba Mngqithi na Chyna Mokaila.
Kwenye nafasi ya kocha wa viungo mashabiki wengi wanatamani kuona Adnan akirejeshwa kwa mara nyingine.
Adnad ndiye aliyeifanya Yanga ya Ramovic itambe kwa muda mfupi kutokana na uwezo wa wachezaji. Timu ilikuwa na kasi kubwa huku wachezaji wakionyesha utimamu wa mwili wa hali ya juu.
Lile soka la Gusa, Achia Twenda Kwao liliwezekana kutokana na umahiri wa Adnad katika eneo la kuwaandaa wachezaji.
Uongozi wa Yanga umeahidi kocha mkuu atatangazwa ndani ya muda mfupi na zipo taarifa kuwepo kwa mawasiliano ya kumpata Ramovic ambaye yuko huru tangu alipoachana na CR Belouizdad.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Adnan ameandika ujumbe mfupi ulioambatana na picha zake mbili zilizopigwa kipindi yupo Yanga. Huenda nae anasubiri wito tu ili arejee Jangwani.
Kwa sasa Yanga inahitaji kumleta kocha ambaye tayari ana uzoefu wa soka la Tanzania na hatahitaji muda mrefu kuiweka timu sawa kwani kiuhalisia muda huu haupo.