Mabingwa watetezi ligi kuu ya NBC Yanga leo wako mkoani Arusha kuikabili TRA United katika mchezo wa kiporo ambao uliahirishwa Oktoba 13.
Ni mchezo ambao Wananchi watahitaji kuchukua alama zote tatu ili kupunguza gap la pointi dhidi ya watani zao Simba ambao wamejisimika kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama sita.
Hata hivyo Yanga inashuka dimba la Sheikh Amri Abeid leo ikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya msimu uliopita ambapo walidondosha alama 2 kwenye uwanja huo.
Presha ni kubwa upande wa Wananchi hasa baada ya kupoteza mchezo dhidi ya watani zao Simba, leo mashabiki wa Yanga wanahitaji matokeo ya aina moja tu, ushindi.
Yanga ilitua Arusha juzi ikiwa na kikosi chake kamili ambapo jana vijana wa kocha Manqoba Mngqithi walikamilisha mandalizi yao kuelekea mtanange huo.
Langoni leo huenda akarejea Djigui Diarra ambaye alikosekana kwenye mechi zilizopita za ligi ya mabingwa kutokana na changamoto ya mgongo.
Hata hivyo Yanga inatarajiwa kuendelea kuwakosa Yao Kouassi na Duke Abuya ambao ni majeruhi huku Stephane Aziz Ki akikamilisha adhabu ya kadi nyekundu.