Manqoba akiri TRA United wagumu, aweka mkakati wa kuwadhibiti

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
1h ago
Manqoba akiri TRA United wagumu, aweka mkakati wa kuwadhibiti

Kocha mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, amekiri kuwa TRA United ni timu yenye ushindani mkubwa na uwezo wa kucheza kwa mbinu mbalimbali, huku akiweka wazi maeneo ambayo kikosi chake kinapaswa kuyadhibiti ili kupata matokeo mazuri katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Yanga inatarajiwa kukutana na TRA United kesho Jumamosi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili.

Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo huo, Mngqithi amesema amepata nafasi ya kuifuatilia TRA United na kuvutiwa na kiwango kizuri ambacho timu hiyo imekuwa ikionesha chini ya kocha wake.

“Nimepata nafasi ya kuifuatilia timu ya TRA na nimevutiwa na kiwango kizuri ilichoonesha chini ya kocha wake. Ni timu yenye ushindani mkubwa, wachezaji wenye uzoefu na uwezo mzuri wa kucheza kwa mbinu mbalimbali,” amesema Mngqithi.

Mipira iliyokufa na mashambulizi ya kushtukiza

Mngqithi amesema Yanga ina kazi kubwa mbele yake na inapaswa kujiandaa kikamilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu uwezo wa wapinzani wao.

Amebainisha kuwa eneo la kwanza ambalo Yanga inapaswa kuwa makini nalo ni mipira iliyokufa, akieleza kuwa TRA United ina nguvu katika kutumia nafasi zinazotokana na mipira hiyo.

Aidha, kocha huyo amesema kikosi chake kinahitaji kuwa na mpangilio mzuri wa ulinzi wakati wa kushambulia ili kuzuia mashambulizi ya kushtukiza ya wapinzani wao.

“Tunapaswa kuwa imara katika mipira iliyokufa kwa sababu ni eneo ambalo wana nguvu. Vilevile, tunahitaji kuwa na mpangilio mzuri wa ulinzi wakati tunaposhambulia ili kuzuia mashambulizi yao ya kushtukiza,” amesema.

Aweka mkakati wa kudhibiti maeneo matatu

Kocha huyo ameeleza kuwa mkakati wa Yanga hautaishia kwenye kuzuia mipira iliyokufa na mashambulizi ya kushtukiza pekee, bali pia utahusisha kuwazuia wapinzani kuanzisha mashambulizi yao kwa uhuru kutoka eneo la nyuma.

Amesema TRA United ina uwezo wa kuanzisha mashambulizi kuanzia kwa mabeki wake, huku kiungo wa ulinzi, namba sita, akitumika mara kwa mara katikati ya mabeki.

Manqoba amesisitiza Yanga inapaswa kuwapa presha wapinzani wake wanapojaribu kujenga mashambulizi kuanzia nyuma, kwa sababu kuwapa nafasi na muda wa kucheza kunaweza kuwawezesha kutumia ubora wao.

“Tukifanikiwa kudhibiti maeneo hayo matatu naamini tunaweza kuwa na nafasi nzuri ya kupata matokeo tunayoyahitaji,” amesema kocha huyo.

Mngqithi ameeleza kuwa TRA United ina kikosi chenye wachezaji wenye uwezo katika maeneo mbalimbali ya uwanja, hali inayowafanya kuwa wapinzani wanaohitaji maandalizi ya kina.

Amesema mabeki wa pembeni wa timu hiyo hupanda kwa nguvu kusaidia mashambulizi, huku mabeki wa kati wakiwa na uzoefu na uwezo mzuri wa kucheza.

Vilevile, amebainisha kuwa safu ya ushambuliaji ya TRA United ina wachezaji hatari wanaoweza kuleta madhara kwa wapinzani, jambo linaloifanya Yanga kuhitaji umakini mkubwa katika kipindi chote cha mchezo.

“TRA ina uwezo wa kuanzisha mashambulizi kuanzia eneo la ulinzi huku kiungo wake wa namba sita akitumika mara kwa mara katikati ya mabeki. Aidha, mabeki wa pembeni ni wachezaji wanaopanda kwa nguvu kusaidia mashambulizi. Mabeki wa kati wana uzoefu na uwezo mzuri, huku safu ya ushambuliaji ikiwa na wachezaji hatari,” amesema.

Manqoba amesema amekiandaa kikosi chake vyema kwa kuzingatia ubora na udhaifu wa wapinzani wake akiwa na imani kuwa kikosi chake kina nafasi ya kuondoka na alama tatu kama watazingatia na kutimiza vyema nkakati waliouandaa kwa ajili ya mchezo huo.

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Manqoba atuma ujumbe kwa wachezaji Yanga 'lazima tupambane kushinda'
Manqoba atuma ujumbe kwa wachezaji Yanga 'lazima tupambane kushinda'
22m ago
READ MORE β†’
Tumejiandaa kushinda dhidi ya TRA United - Masalanga
Tumejiandaa kushinda dhidi ya TRA United - Masalanga
36m ago
READ MORE β†’
Yanga yapania alama tatu Arusha
Yanga yapania alama tatu Arusha
3h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Ijumaa, Oktoba 23 2026
Magazeti ya leo Ijumaa, Oktoba 23 2026
6h ago
READ MORE β†’
Manqoba tunamuamini - Kamwe
Manqoba tunamuamini - Kamwe
20h ago
READ MORE β†’
Kituo kinachofuata ni TRA United
Kituo kinachofuata ni TRA United
23h ago
READ MORE β†’
Karibu tena dimbani Job
Karibu tena dimbani Job
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Alhamisi, Oktoba 22 2026
Magazeti ya leo Alhamisi, Oktoba 22 2026
1d ago
READ MORE β†’
Highlights; Yanga 4-1 CFFA, CAFCL (FT)
Highlights; Yanga 4-1 CFFA, CAFCL (FT)
1d ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 4-1 CFFA, CAFCL (FT)
FT : Yanga 4-1 CFFA, CAFCL (FT)
1d ago
READ MORE β†’