Mashabiki wa Yanga wanahesabu saa kabla ya kuelekea uwanja wa Uhuru kushuhudia mchezo wa dabi ya Kariakoo wakati timu yao itakapokuwa ikimenyana na Simba katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Mtanange huo wa kukata na shoka unatarajiwa kupigwa kuanzia saa 1 usiku, Yanga wakiwa ugenini.
Yanga inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa katika nyakati nzuri kwani wachezaji wote wako tayari.
Mkufunzi wa Yanga Manqoba Mngqithi amekiandaa kikosi chake kikamilifu akiahidi kuwadhiiti Simba katika maeneo ambayo wamekuwa wakiyatumia kufunga mabao.
Manqoba alisema timu hiyo imekuwa ikitumia zaidi mipira iliyokufa kufunga mabao ambapo kati ya mabao 11, mabao 7 wamefunga kupitia aina hiyo ya mpira.
Mawinga wao Anicet Oura na Libasse Gueye ndio wanaonekana kuhusika zaidi kwenye kusababisha mabao hayo hasa Libasse ambaye amehusika kwenye mabao 6 yaliyofungwa na timu hiyo.
Manqoba amewaandaa walinzi wake wa pembeni Yao Kouassi na Chadrack Boka kuhakikisha hakuna madhara yanayosababishwa na wachezaji hao kwenye maeneo yao.

Yao na Boka wamethibitisha kwenye mechi zilizopita dhidi ya Simba wakifanikiwa kuwadhibiti wachezaji hao wa pembeni, leo watahitaji kufanya tena jukumu hilo kwa ufanisi.
Lakini pia eneo la ushambuliaji la Yanga linalotarajiwa kuongozwa na Peter Shalulile linapaswa kuwa na ukatili kwa kutumia nafasi zitakazotengenezwa.
Manqoba amesema hana wasiwasi na utengenezaji wa nafasi kwenye kikosi chake, amekuwa akifanya kazi kwenye uwanja wa mazoezi ili kuwaongezea washambuliaji wake ufanisi kwenye matumizi ya nafasi hizo.
Amesema ipo siku kuna timu italipa gharama ya idadi ya nafasi ambazo wamekuwa wakizipoteza, anaamini siku hiyo timu yake itafunga mabao mengi.
Je siku hiyo inaweza kuwa leo? Itafahamika pale uwanja wa Uhuru saaa 1 usiku...!