Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema Uwanja wa Uhuru uliopo jijini Dar es Salaam upo tayari kwa mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya wenyeji, Simba SC dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC utakaofanyika Oktoba 10, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara mapema leo, uwanja huo hautatumika kwa mazoezi na timu yoyote kati ya hizo mbili. Wizara imesisitiza kwamba kanuni na taratibu zilizowekwa na Bodi ya Ligi kuhusu matumizi ya uwanja wa mashindano, hususani masuala yanayohusu mazoezi ya timu, zizingatiwe kikamilifu.
“Hivyo basi, ifahamike kua kuelekea mchezo huo Uwanja wa Uhuru hautatumika kwa mazoezi na timu yoyote kati ya hizo mbili, kwa kuzingatia matakwa ya kifungu husika cha kanuni za mashindano ya ligi.”
“Tunawaomba wadau wote, mashabiki wa Simba na Yanga, pamoja na umma kwa ujumla, kuzingatia utulivu, amani na taratibu zilizowekwa kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na Watanzania wote.” imesema taarifa ya Wizara