Kikosi cha Yanga Princess leo mchana kitashuka uwanja wa KMC Complex kuikabili Mashujaa Queens katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Ngao ya Jamii Wanawake.
Yanga Princess ilipoteza mchezo wa nusu fainali dhidi ya Simba Queens kwa kuchapwa mabao 3-0 wakati Mashujaa Queens walipoteza nusu fainali dhidi ya JKT Queens kwa kufungwa bao 1-0.
Kocha Msaidizi wa Yanga Princess Said Maulid 'SMG' amesema baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba Queens, wanataka heshima angalau ya kumaliza nafasi ya tatu.
Amesema wanatambua ubora wa Mashujaa Queens lakini wamejipanga kukabiliana nao.
SMG amesisitiza kuwa msimu huu wana matarajio makubwa kwa kikosi cha Yanga Princess kutokana na maboresho waliyofanya wakiongeza wachezaji wengi ambao ni vijana wenye ari na nguvu ya kupambana.
Mchezo huo wa kusaka mshindi wa tatu unatarajiwa kupigwa saa 7 mchana.