Baada ya mapumziko ya siku nane kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea mazoezini kuanza maandalizi ya mikiki mikiki ya ligi kuu, ligi ya mabingwa mwezi Oktoba.
Kwa mujibu wa ratiba, katika kipindi cha siku 20 Yanga inatarajiwa kucheza mechi tano, katika mashindano yote.
Unaweza kusema kocha Manqoba Mangqithi atakuwa na jukumu la kuhakikisha anaivusha Yanga salama katika mechi tatu muhimu mwezi Oktoba.
Mechi ya kwanza ni dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba itakayopigwa Oktoba 10. Huu ni mchezo ambao Yanga inalenga kuendeleza ubabe wake dhidi ya watani zao.
Imani ya mashabiki wa Yanga ni kuhakikisha timu yao haipoteza mchezo huu ili kuendelea kulinda nafasi yao kileleni mwa msimamo wa ligi.
Lakini pia kutakuwa na mechi mbili za kuamua hatma ya Yanga kucheza hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL).
Katika hatua hiyo Yanga itaumana na CFFA ya Madagascar ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza utapigwa Oktoba 17 nchini Mauritius na mchezo wa marudiano kupigwa wiki moja baadae jijini Dar es salaam.
Malengo ya Yanga kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu ni angalau kufika robo fainali ingawa Manqoba ameweka malengo makubwa zaidi ya kuwania taji hilo.
Pia kutakuwa na mechi za ligi kuu dhidi ya TRA United (Oct 13, ugenini) na Mashujaa Fc (Oct 27, nyumbani).