Nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachokabiliana na Simba katika Dabi ya Kariakoo Oktoba 10, lakini amesema hana hofu na uwezo wa timu yake kufanya vizuri licha ya kukosekana kwake.
Aziz Ki alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Geita Gold kufuatia tukio lililomhusisha mchezaji wa timu hiyo, Datius Peter, hatua iliyomfanya akabiliwe na adhabu ya kukosa michezo miwili.
Hivyo, kiungo huyo atalazimika kuikosa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba, huku mchezo huo ukiwa wa kwanza katika michezo miwili atakayotumikia adhabu hiyo. Mchezo unaofuata ambao pia ataukosa ni dhidi ya TRA United.
Awali, Yanga iliwasilisha malalamiko kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ikiomba kadi hiyo ifutwe kwa madai kuwa Aziz Ki hakukusudia kumuumiza Datius Peter.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa taarifa ya Kamati ya Saa 72, hakuna kilichobadilika na sasa mchezaji huyo atalazimika kutumikia adhabu ya michezo miwili.
Aziz Ki, ambaye amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa Yanga katika misimu ya nyuma, amesema kikosi cha timu hiyo hakimtegemei mchezaji mmoja na kwamba yeyote atakayepewa nafasi ana uwezo wa kufanya kazi nzuri kwa ajili ya timu.
“Ninaamini kwenye kikosi chetu. Yanga ina wachezaji wengi wazuri na kila mmoja ana uwezo wa kuisaidia timu. Mimi sitakuwepo, lakini naamini wenzangu watafanya kazi nzuri,” alisema Aziz Ki.
Kiungo huyo alisema kinachomuumiza zaidi ni kukosa mchezo huo wenye uzito mkubwa kwa mashabiki wa timu hizo mbili, lakini licha ya kutokuwepo uwanjani, ataendelea kuwaunga mkono wachezaji wenzake.
“Nitakuwa pamoja nao kwa moyo. Natamani ningekuwa uwanjani kusaidia timu, lakini kwa kuwa sitakuwepo, nitawaunga mkono na kuamini watafanya vizuri,” alisema.