Taifa limeingia katika majonzi mazito kufuatia kifo cha aliyekuwa mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, aliyefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 97, ikiwa ni miaka 54 tangu kuuawa kwa mumewe, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1972.
Msiba huo umepokelewa kwa simanzi kubwa huku viongozi mbalimbali na wadau wa soka nchini wakikumbuka mchango mkubwa wa Familia ya Karume katika historia ya ujenzi wa nchi na sekta ya michezo, hususan klabu kongwe ya Yanga SC.
Enzi za uhai wake, Mama Fatma alizaliwa mwaka 1930 huko Bumbwini, Unguja, na kufunga ndoa na Mzee Karume mnamo Novemba 1944. Alikuwa nguzo imara na mfano wa kuigwa wa malezi, akimlea pia Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Wakati nchi ikimlilia mwanamke huyo shujaa, wadau wa soka wameitumia fursa hii kuamsha kumbukumbu za mumewe, Sheikh Abeid Amani Karume, ambaye anatajwa kuwa mmoja wa waasisi na walezi wakuu wa soka la kisasa nchini kupitia klabu ya Yanga.

Historia inaonyesha kuwa Mzee Karume alikuwa mwanachama na mpenzi mkubwa wa Yanga tangu enzi za ujana wake alipokuwa akifanya kazi kama baharia.
Uhusiano wake wa karibu na klabu hiyo ulifikia kilele mnamo mwaka 1971, pale alipoguswa na changamoto za miundombinu zilizokuwa zikiikabili klabu hiyo.
Katika kile kinachotajwa kama mapinduzi makubwa ya soka, Mzee Karume alitoa msaada wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la makao makuu ya Yanga na uwanja wao wa mazoezi uliopo Jangwani, ambao baadaye ulikuja kujulikana kama 'Uwanja wa Kaunda'. Ni katika eneo hilo Yanga inajenga uwanja wake mpya.
Hatua hiyo ilimfanya kuwa kiongozi wa kwanza serikalini kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye klabu ya soka.Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanabainisha kuwa Mzee Karume hakuwa na ubaguzi; licha ya mapenzi yake kwa Yanga, alihakikisha pia wapinzani wao wakubwa, Simba SC (wakati huo Sunderland), wanapata jengo lao la mtaa wa Msimbazi na kuwa mhimili wa kubadili jina lao la kikoloni.
Kifo cha Mama Fatma Karume kimefunga ukurasa muhimu wa mashuhuda wa historia ya muungano na uasisi wa soka letu, lakini alama zilizochorwa na familia yake kwenye mioyo ya WanaYanga na Watanzania kwa ujumla zitabaki daima.
Buriani Mama Karume..