Kocha Mkuu wa klabu ya St. George ya Ethiopia, Milutin Sredojevi ‘Micho’, ameimwagia sifa klabu ya Yanga baada ya mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki, huku akiwatabiria mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara kufanya makubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAFCL) msimu huu.
Kauli hiyo ya Micho inakuja kufuatia mchezo mkali wa kirafiki uliopigwa jana Ijumaa, ambapo Yanga iliondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Waethiopia hao, mchezo uliotumiwa na timu zote mbili kama sehemu ya maandalizi na kujiimarisha.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mtanange huo, kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika alikiri kuwa Yanga kwa sasa ina kikosi imara na chenye ushindani wa hali ya juu ambao utawasaidia kufika mbali kimataifa.
"Yanga ni timu imara sana kwa sasa. Nawatabiria kufika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Wana ubora, muundo na wachezaji wenye uwezo wa kushindana na timu yoyote kubwa barani Afrika," alisema Micho.
Mbali na pongezi hizo, Micho alifafanua kuwa mchezo huo umekuwa na faida kubwa kwa kikosi chake ambacho kwa sasa kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi. Alieleza kuwa kupoteza mbele ya Yanga kumesaidia vijana wake kupata somo na uzoefu mkubwa wa kimataifa utakaowajenga kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Ethiopia.
Kwa upande wa benchi la ufundi la Yanga, linaloongozwa na kocha Manqoba Mngqithi, walieleza kupokea ushindi huo kwa mikono miwili huku wakifurahia kiwango cha jumla kilichoonyeshwa na wachezaji wao.
Hata hivyo, walibainisha kuwa bado wana kazi ya kufanya katika safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha wanazitumia vyema nafasi zinazopatikana kwenye mechi za ushindani mkubwa.