Yanga imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya St George katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Uhuru.
Ulikuwa mchezo wa kiufundi zaidi ambao uliwapa makocha wa timu zote nafasi ya kujaribu mifumo na wachezaji hasa wale ambao hawakupata nafasi ya kutumika zaidi kwenye mechi zilizopita.
Yanga ilitawala mchezo huo kwa muda mwingi huku vijana wa Micho wakijilinda kwa nidhamu ya hali ya juu.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana. Hata hivyo Yanga ilifanikiwa kupata bao pekee la ushindi kwenye kipindi cha pili likiwekwa kimiani na Albert Kangwanda akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Maxi Nzengeli ambaye leo alivaa kitambaa cha unahodha.
Kwenye mchezo huo Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi aliendelea na utaratibu wake wa kufanya majaribio akimtumia Yao Kouassi katika eneo la kiungo.
Ulikuwa mchezo wa urafiki baina ya timu hizo ambazo zote zimetimiza miaka 91 mwaka huu.

