Hamasa kuelekea kilele cha tamasha la kila mwaka la Wiki ya Wananchi inazidi kupamba moto Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe, akianza mapema mazoezi ya kushangilia mabao ya mshambuliaji Peter Shalulile.
Kamwe amewaasa mashabiki na wanachama wa Yanga kuchangamkia tiketi zao mapema na kufurika kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru siku ya Jumapili, Agosti 9, 2026.
Tamasha hili la msimu huu, linalojulikana pia kama Yanga Day, linatarajiwa kuwa la kihistoria kwani mashabiki watapata fursa ya kwanza ya kumshuhudia Peter Shalulile akiwa na mastaa wengine wakiwa ndani ya uzi wa kijani na njano.
Kwa jinsi Yanga mpya inavyoogopesha, Kamwe amefichua kuwa hata baadhi ya timu walizokuwa wakizungumza nazo kwa ajili ya mchezo wa kirafiki "zimeingia mitini" kwa hofu ya kukutana mapema na kikosi cha kocha Manqoba Mngqithi.
Tamasha hilo litaanza majira ya saa 4:00 asubuhi likihusisha burudani za wasanii wakubwa, utambulisho wa kikosi kizima na benchi la ufundi la msimu wa 2026/2027, na litarushwa mbashara kupitia Azam TV.Β

