Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema shirikisho limefanya maboresho ya kanuni za mashindano kwa lengo la kuimarisha nidhamu na kuhakikisha haki inatendeka katika soka la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari za michezo katika Ofisi za TFF, Karia alisema kuwa kuanzia sasa timu yoyote itakayobainika kutumia vyumba vya kubadilishia nguo visivyo rasmi bila sababu za msingi itakabiliwa na adhabu kali ya kupokonywa pointi tano, hata kama itakuwa imeshinda mchezo husika.
Karia alieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kuwepo kwa matukio yanayokiuka taratibu za matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo, hali inayoweza kuathiri uadilifu wa mashindano.
Mbali na kurekebisha kanuni, TFF pia imeandaa vifaa maalum vitakavyowekwa katika vyumba vya kubadilishia nguo ili kusaidia kudhibiti vitendo visivyokubalika, ikiwemo matumizi ya gesi au mazingira yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama na afya ya wachezaji pamoja na viongozi wa timu.
Alisisitiza kuwa endapo uchunguzi utathibitisha kuwa timu ilitumia chumba tofauti na kilichotengwa na uwanja bila sababu za msingi au dharura, hatua za kinidhamu zitachukuliwa mara moja kwa mujibu wa kanuni mpya.