Nyota waliokuwa majeruhi Dickson Job na Clement Mzize jana walijumuika na wachezaji wengine katika siku ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya 2026/27.
Kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa na Yanga, ni kuwa wachezaji hao wako chini ya uangalizi kabla ya kurejea rasmi kwenye majukumu yao kikamilifu.
Hata hivyo kuna dalili njema za kuimarika hasa mshambuliaji Clement Mzize ambaye alionekana kuwa imara akishiriki kikamilifu program za mazoezi chini ya kocha Manqoba Mangqithi. Mzize anaweza kurejea mapema kikosini tofauti ya ilivyotarajiwa.
Wakati Job akipata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Simba March 1 mwaka huu, Mzize amekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na changamoto ya jeraha la goti.
Msimu uliopita alitumika kwa muda mfupi mechi za hatua ya awali ligi ya mabingwa lakini akatonesha majeraha ambayo alipata wakati akiitumikia timu ya Taifa kwenye michuano ya CHAN 2024.
Akarejea tena katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS FAR ugenini lakini akatonesha tena jeraha wakati wa maandalizi ya mchezo dhidi ya JS Kabylie.
Baada ya kuumia kwa mara ya pili, uongozi wa Yanga ulilazimika kumpeleka Afrika Kusini kupata matibabu zaidi mwezi Februari 2026 ambapo tangu wakati huo ameendelea kuimarika taratibu.
Sasa yuko kwenye awamu ya mwisho ya kuimarisha eneo lililopata changamoto na kurejesha fitness ya mwili kabla ya kuanza rasmi kuonekana kwenye mechi za ushindani.


