Mkurugenzi wa kampuni ya SportPesa Abbas Tarimba ameipongeza klabu ya Yanga kwa kufanikiwa kushinda mataji matano mfululizo ya ligi kuu ya NBC.
Akizungumza jana baada ya Yanga kuwasilisha makombe hayo Makao Makuu ya kampuni hiyo, Tarimba alisema mafanikio hayo ni faraja kwao kwani udhamini wao umekuwa na mchango chanya kwa Yanga.
“Nawashukuru sana Yanga SC kwa ziara yao ya makombe hapa ofisini kwetu. Sisi kama Sportpesa tunajivunia sana kuwa sehemu mafanikio makubwa ambayo Yanga imepata. Yanga ndio timu ambayo tumeidhamini kwa kipindi kirefu sana. Katika kipindi hiki Yanga imeweka rekodi ya kunyakua mataji matano mfululizo. Haya ni mafanikio makubwa sana”
“Yanga ni timu ambayo tumeidhamini kwa kipindi kirefu sana na uhusiano wetu haujajengwa kwenye udhamini pekee, bali kwenye imani, mshikamano na ndoto ya kuona klabu hii ikiendelea kukua na kufika mbali zaidi. Haya si mafanikio ya kawaida; yanaonyesha uimara wa taasisi, mipango bora na utamaduni wa ushindi ambao umejengwa ndani ya klabu,” alisema.
SportsPesa imekuwa wadhamini wakuu wa Yanga kwa takribani miaka 9 sasa wakiingia kwa mara ya kwanza mwaka 2017.



