Wakati msimu ukielekea ukingoni kulikuwa na tetesi kuwa Yanga ingeachana na mshambuliaji wake Laurindo Aurelio 'Depu' lakini sasa ni wazi Depu ataendelea kusalia Jangwani.
Katika mechi za mwishoni mwa msimu, Depu alidhihirisha kwa nini Rais wa Yanga Injinia Hersi Said alimfuata Ulaya kumrejesha Afrika baada ya mapendekezo ya aliyekuwa kocha wa Yanga Pedro Goncalves anayetarajiwa kutua AS FAR kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Licha ya kutua Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo, Depu amepachika mabao 9 kwenye ligi, mabao mawili ligi ya mabingwa na mabao matatu kombe la Shirikisho la CRDB akifunga jumla ya mabao 14 kwenye mashindano yote.
Ikumbukwe mshambuliaji huyo alikosa mechi nyingi kutokana na majeraha na wakati mwingine akipata dakika chache kwenye baadhi ya mechi.
Usajili wake pamoja na kiungo Mganda Allan Okello ulikuwa na thamani kubwa kwa Yanga kwani tangu watue kwa Wananchi mchango wao ni mkubwa.
Inaelezwa tayari Yanga imemsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Yves Koutiama anayechukua nafasi iliyoachwa na Prince Dube.
Koutiama anatua Yanga akitokea klabu ya Polisi Fc ya Kenya aliyojiunga nayo kwenye usajili wa dirisha dogo.
Koutiama na Depu huenda wakawa washambuliaji viongozi msimu ujao huku Clement Mzize nae akitarajiwa kurejea baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na majeraha.