Kiungo wa Kimataifa wa Uganda Khalid Aucho amefikia makubaliano ya pande mbili na uongozi wa Singida BS akiachana na walima alizeti hao baada ya kuwatumikia kwa msimu mmoja.
Aucho alitua Singida BS msimu uliopita akitokea klabu ya Yanga akisaini mkataba wa miaka mwili.
Hata hivyo msimu mmoja umetosha kwake kuondoka huku mashabiki wakisubiri kuona kituo chake kinachofuata.
Wakati Aucho akiondoka Singida BS, Yanga iko sokoni kusaka kiungo mkabaji huku kukiwa na maoni tofauti miongoni mwa mashabiki ambapo wapo wanaotamani kuona kiungo huyo akirejea Jangwani.
Lakini pia wapo wengine wanaamini misimu mitatu aliyowatumikia Wananchi imetosha kwani umri nao unamtupa mkono.
Wakati anaondoka Yanga Aucho aliweka wazi kuwa yeye ataendelea kuwa Mwanafamilia wa Yanga akiamini anaweza kurejea katika klabu hiyo hata kwa majukumu mengine.
Yanga ilimuandalia Aucho tuzo maalum ya kutambua mchango wake mkubwa akishiriki kikamilifu kuirejesha Yanga kwenye ushindani na kutwaa mataji.

Ni miongoni mwa wachezaji walioleta 'mapinduzi' Yanga baada ya kusajiliwa na GSM akitua na nyota wengine kama Djigui Diarra, Fiston Mayele, Jesus Moloko, Yannick Bangala, Djuma Shaban na Heritier Makambo ambaye alirejeshwa kwa mara ya pili akitokea Horoya Ac.
Ni katika msimu huo 2021/22 Yanga ilianza kushinda mataji mfululizo na kurejesha ufalme wake kwenye soka la ndani.