Mabingwa wa soka Tanzania Bara kwa misimu mitano mfululizo, Yanga SC, wameanza harakati za kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu mpya, huku jina la winga hatari Jean Claude Girumugisha likiendelea kutawala viunga vya Twiga na Jangwani.
Licha ya dau kubwa la usajili linalodaiwa kuzidi Shilingi bilioni 3 ambalo limewekwa na klabu ya Al Hilal Omdurman ili kumuachia nyota huyo, taarifa zinaeleza kuwa Yanga bado haijakata tamaa na inaendelea kutafuta njia ya kufanikisha dili hilo.
Rais wa Yanga, Hersi Said, tayari ameweka wazi dhamira ya klabu hiyo kufanya usajili mkubwa katika dirisha hili la usajili, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya timu kuwa na ushindani mkubwa zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Harakati za Yanga zimeongezeka baada ya kupata pigo kubwa mnamo Juni 30, kufuatia kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua kupata majeraha makubwa yanayoweza kumuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo, mabosi wa klabu hiyo wanaendelea kufanya tathmini ya kumpata mchezaji mwenye uwezo wa kuziba pengo hilo, au hata kuongeza ubora zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Ndani ya mipango hiyo, Jean Claude Girumugisha ameendelea kuwa jina linalojirudia mara kwa mara katika vikao vya usajili vya Yanga. Winga huyo mwenye kasi, ubunifu na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi pamoja na kufunga mabao, sifa ambazo zinaendana na falsafa, mahitaji ya Yanga.
Girumugisha ni miongoni mwa wachezaji chipukizi wanaovutia zaidi kwa sasa barani Afrika. Bado ana mkataba wa muda mrefu na klabu ya Al Hilal Omdurman, ambako ameendelea kuonyesha kiwango bora, hususan katika mashindano ya CAF. Kiwango hicho kimechangia kupanda kwa thamani yake katika soko la usajili na kufanya dili lake kuwa gumu zaidi.
Hata hivyo, Yanga inaonekana kuwa tayari kufanya uwekezaji mkubwa ili kupata saini ya nyota huyo, ikiwa itaamini ndiye mchezaji sahihi wa kuiongoza timu kuelekea mafanikio mapya msimu ujao.
Iwapo usajili huo utafanikiwa, Girumugisha anaweza kuwa miongoni mwa usajili mkubwa zaidi katika historia ya Yanga, huku ukitoa ujumbe kwamba mabingwa hao wa Tanzania wana nia ya kujenga kikosi chenye uwezo wa kushindana kwa kiwango cha juu katika mashindano ya Afrika.