Kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc, Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin na benchi la ufundi wana kazi ya kuhakikisha yale makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita wa nusu fainali ya kombe la CRDB hayajirudii tena siku ya kesho kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc.
Juzi Yanga ilipoteza mchezo wa nusu fainali kwa kufungwa mabao 3-2 huku Azam Fc wakifunga mabao yote kupitia mipira ya kichwa.
Ukiacha bao la tatu ambalo lilitokana na makosa ya beki Ibrahim Bacca, mabao mengine mawili yalitokana na kukosekana umakini kwenye kucheza mipira ya krosi.
Ukiwafuatilia Azam Fc, wanafanya sana mazoezi ya kumaliza mipira iliyokufa yaani kona na faulo, ikionyesha ndio silaha ambayo wamelenga kuitumia kwenye mchezo huo.
Ni kwa sababu Yanga ilionyesha udhaifu mkubwa kuondoa mipira ya krosi. Hili ni tatizo ambalo limekuwa likiisumbua Yanga kwa muda mrefu ingawa kipindi cha karibuni ni kama walipata dawa ya kukabiliana na mipira ya aina hiyo.
Jumatano Azam Fc wanatarajiwa kuwekeza zaidi kwenye mipira ya aina hiyo, hivyo Moalin na vijana wake wanapaswa kuwa tayari kukabiliana nayo.