Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC, wamerejea kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha. Ushindi huo umeendelea kuonyesha ubora wa kikosi hicho katika mbio za kutetea ubingwa wao wa ligi.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya bila kufungana, Yanga walirejea uwanjani kwa kasi zaidi katika kipindi cha pili na kufanikiwa kupata mabao mawili yaliyowahakikishia pointi tatu muhimu.
Kiungo Pacôme Zouzoua aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 53 kabla ya mshambuliaji Depú kuongeza la pili dakika ya 55 na kuzima kabisa matumaini ya Fountain Gate kurejea mchezoni.
Katika mchezo huo, Yanga walionyesha nidhamu kubwa ya kiuchezaji pamoja na umiliki mzuri wa mpira, hali iliyowapa nafasi ya kutawala sehemu kubwa ya mchezo dhidi ya wapinzani wao waliokuwa wakicheza mbele ya mashabiki wao.
Ushindi huo umeifanya Yanga kukusanya pointi muhimu na kufikisha alama 66 na kuwaondoa watani zao Simba juu ya msimamo wakikaa hapo kwa takribani saa 24
Yanga sasa inahitaji kushinda angalau mechi mbili na sare moja ili kutetea ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo.
Mechi tatu zilizobaki ni dhidi ya Azam Fc, TRA United na JKT Tanzania.

