Yanga imechukua alama zote tatu mkoani Kigoma ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Alikuwa ni Mudathir Yahya aliyeifungia Yanga bao la kwanza kwenye dakika ya 28 kwa shuti la nje ya 18 akimalizia pasi ya Prince Dube.
Pengine Yanga ilipaswa kumaliza mchezo huo kwenye kipindi cha kwanza kwani walitengeneza nafasi zaidi Maxi Nzengeli na Dube wakipoteza nafasi mbili adimu.
Kipindi cha pili Yanga ilipunguza kasi na kuwapa Mashujaa Fc nafasi ya kutawala mchezo huku Wananchi wakitumia mashambulizi ya kujibu.
Wakati ikionekana mchezo huo ungemalizika kwa Yanga kushinda moja, shambulizi kali dakika za lala salama lilipelekea bao la pili la Yanga likifungwa na nahodha Bakari Mwamnyeto.
Ushindi huo unaifanya Yanga ijiimarishe kileleni mwa msimamo wa ligi sasa kwa tofauti ya alama tano dhidi ya watani zao Simba ambao watacheza dhidi ya Pamba Jiji Jumpili.