Klabu ya Yanga inatajwa kuwa kwenye mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji Yves Koutiama (27) raia wa Burkina Faso.
Kwenye msimu uliomaliza, Koutiama aliitumikia timu ya Polisi Fc ya Kenya akiungana na timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo.
Mfumania nyavu huyo aliweka kambani mabao 10 na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa kigeni licha ya kuitumikia Polisi Fc kwa muda mfupi.
Yanga imedhamiria kufanya maboresho kwenye safu ya ushambuliaji, Koutiama anaonekana kukidhi vigezo.
Mshambuliaji huyo ameandaliwa mkataba wa miaka miwili, ambapo mazungumzo yanatajwa kuwa kwenye hatua za mwisho.
Kabla ya kutua Polisi Fc, Koutiama aliitumikia klabu ya USFA Ouagadougou ya kwao Burkina Faso.
Kwenye mechi yake ya kwanza tu baada ya kutua Polisi Fc mwezi Januari, aliweka kambani mabao mawili na akaendelea kuzifumania nyavu na kumaliza msimu akifunga mabao 10.