Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin amesema mapumziko ya kalenda ya FIFA yamewasaidia wachezaji na sasa wamerejea wakiwa na nguvu mpya kwa ajili ya kumalizia kwa nguvu mechi zilizosalia.
Yanga ilirejea mazoezini juzi baada ya mapumziko ya wiki moja wachezaji wakifanya 'session' mbili za mazoezi kila siku ukiwa ni mkakati wa kuwaweka tayari kwa mikiki mikiki ya mchi za kumaliza msimu.
Moalin ambaye anashirikiana na Patrick Mabedi wakipewa jukumu la kuhakikisha Yanga inatetea mataji yake mawili, amesema ratiba ya ligi imekuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa, hivyo mapumziko hayo yalikuwa muhimu kwa wachezaji kuurejesha utimamu wa mwili na kujiandaa kwa changamoto zilizobaki.
“Tuliwapa wachezaji muda mzuri wa kupumzika. Lengo lilikuwa kupumzisha miili yao na kuhakikisha wanarudi wakiwa na nguvu mpya kwa ajili ya mechi zilizobaki”
“Yanga imejikita katika kumalizia kwa nguvu mechi tano zilizosalia za ligi huku kila mmoja ndani ya kikosi akitambua umuhimu wa kupata matokeo mazuri katika hatua hii ya mwisho ya msimu,” amesema Moalin
Yanga wataanzia mkoani Kigoma kampeni ya kuwania alama 15 za ubingwa kwa mchezo dhidi ya Mashujaa Fc utakaopigwa Juni 13 uwanja wa Lake Tanganyika.