Jioni ya leo majira ya saa 12:30 Yanga itakuwa uwanja wa KMC Complex kumenyana na Namungo Fc katika mwendelezo wa ligi kuu ya NBC.
Ni mchezo ambao Yanga itaingia ikiwa na dhamira moja tu, kusaka ushindi ili irejee kileleni mwa msimamo wa ligi.
Lakini pia mashabiki wa Yanga wanatarajiwa kufurika pale KMC Complex kumshuhudia Star Boy Allan Okello ambaye amekuwa katika kiwango kizuri cha ufungaji katika mechi za karibuni.
Okello ameweka rekodi ya aina yake ya kufunga mabao katika mechi nne mfululizo huku mechi 3 akifunga mabao mawili kwenye kila mechi.
Aliwapiga KMC bao 1, kisha akazifunga Coastal Union, Dodoma Jiji na Singida BS mabao mawili. Yaani katika mechi nne pekee Okello amefunga mabao 7 huku pia akihusika kwenye mabao mengine 7 ambayo ametoa asisti.
Lakini pia urejeo wa Mudathir Yahya kikosini umeongeza uhakika wa mabao kwani tangu amalize adhabu ya kufungiwa mechi tatu, tayari amepachika mabao mawili.
Muda ana mabao 8 kwenye ligi akiwa nyuma ya Okello na Prince Dube kwa tofauti ya bao moja tu, wawili hao wanaongoza kwa kuzifumania nyavu kwenye kikosi cha Yanga kila mmoja akifunga mabao 9.