Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin amesema licha ya muda finyu wa maandalizi, kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa kesho Jumtatu katika uwanja wa KMC Complex.
Moalin amesema wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa mchezo huo na wataweka nguvu katika mechi zao zaidi bila ya kujali matokeo ya wapinzani wao.
“Maandalizi ya mchezo wetu wa kesho dhidi ya Namungo yanaendelea vizuri, tuna muda mchache lakini tuna matumaini makubwa. Namungo ni timu ngumu lakini kipaumbele chetu ni alama tatu, sitaki kuongelea sana uwiano wa alama na mpinzani yoyote. Mikakati yetu ni kushinda kila mechi”
“Tunatambua umuhimu wa kila mchezo, hatuogopi kufanya kazi katika mazingira yenye presha. Tunacheza kama tunavyocheza siku zote, sisi ni Yanga. Tunahitaji presha ili kutusukuma mbele zaidi, kitu cha muhimu ni alama tatu hakuna kitu kingine. Hatuwezi kupangia wenzetu wacheze vipi sisi tuna malengo yetu”
“Kila mchezaji anajua mashabiki na timu inataka nini, tuna matarajio kuwa kila mchezaji yupo tayari kwa mapambano. Pacome alipata majeraha kidogo mchezo uliopita lakini anaendelea vizuri, wachezaji wengine wapo sawa kimwili na kiakili. Lakini pia tunahitaji hamasa ya kutosha kutoka kwa mashabiki. Nawasihi mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi,” alisema Moalin
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, mlinda lango Aboutwalib Mshery amesema wanatambua ugumu wa mchezo dhidi ya Namungo Fc huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.
“Tunafahamu mchezo unaokuja utakuwa mgumu sana kutokana na nafasi waliyopo Namungo. Namungo ni timu nzuri na tunawaheshimu, lakini mchezo ambao upo mbele yetu ni fainali. Ratiba imekuwa ngumu lakini hatuna budi, kupambania kila alama tatu ambazo zipo mbele yetu”
“Uwepo wa mashabiki uwanjani ndio chachu ya ushindi wetu. Kila shabiki wa Yanga anatambua umuhimu wa uwepo wa mashabiki uwanjani. Shabiki ni mchezaji wa 12 ambaye kazi yake ni kutupatia nguvu na hamasa tunapokuwa tunapambana uwanjani. Tunaomba sana wajitokeze kwa wingi, huu ndio wakati tunamuhitaji sana shabiki uwanjani kuliko kitu chochote,” alisema Mshery