Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe ametoa ufafanuzi kwa kile kilichoonekana kama sintofahamu kati ya mlinda lango Djigui Diarra na nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwanyeto katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji ambao Yanga walishuhudia unbeaten ya mechi 42 ikifika mwisho kwa kipigo cha mabao 3-2.
Akizungumza jijini Dar es salaam mapema leo baada ya kikosi cha Yanga kurejea Dar wakitokea Dodoma, Kamwe amesema tukio lililotokea ni mambo ya kawaida na kuwa jambo hilo liliishia pale pale uwanjani.
"Hakuna sintofahamu yoyote baina ya wachezaji wetu Diarra na Mwamnyeto. Kila mchezaji anapokuwa uwanjani lengo lake ni kuipambania timu hivyo masuala ya kupishana kauli ni jambo la kawaida kabisa kwa wachezaji wanapokuwa kwenye majukumu yao."
"Lakini mambo hayo yanaishia palepale uwanjani niwahakikishie kuwa hakuna tofauti yoyote, " alisema Kamwe
Yanga imerejea Dar leo wakitokea Dodoma ambapo watakuwa na siku mbili za maandalizi kuelekea mchezo wa robo fainali kombe la CRDB dhidi ya JKT Tanzania.