Inaelezwa uongozi wa Yanga umekamilisha mazungumzo ya kumuongeza mkataba mshambuliaji kinara Prince Dube, imefahamika.
Dube ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao na Yanga inamalizika mwishoni mwa msimu.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani zinaeleza kuwa, pande zote mbili zimefikia makubaliano kamili, huku kilichobaki kikiwa ni hatua ya mwisho ya kusaini mkataba huo, hatua inayotarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia sasa.
Uongozi wa Yanga umefikia hatua ya kumuongeza Dube mkataba baada ya kuridhishwa na kazi anayoifanya akifunga na kutoa pasi za mabao.
Dube ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi cha Yanga akiwa amefunga mabao 9 kwenye ligi na kutoa pasi nne za mabao.
Anashirikiana vyema na mshambuliaji mwenzake Laurindo Aurelio 'Depu' ambaye amerejea hivi karibuni kikosini baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa wiki kadhaa.
Depu aliyejiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo Januari, amefunga mabao 6 kwenye ligi na kutoa pasi moja ya bao.