Unaweza kusema Yanga 'wanautaka' mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba utakaopigwa Jumapili May 03 katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Jijini Dar es salaam.
Baada ya kupoteza mchezo wa fainali kombe la Muungano dhidi ya Simba juzi, hakukuwa na muda wa kupoteza kwani jana kikosi kilirejea mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya kuikabili Simba kwa mara ya pili katika kipindi cha siku tano.
Ari na morali ya wachezaji iko juu, nyuso zao zikionyesha ni kwa kiasi gani hawakufurahia kupoteza mchezo dhidi ya watani zao tena kwenye dakika za lala salama.
Mchezo wa May 03 ndo wenye umuhimu mkubwa kwani matokeo ya ushindi kwa Wananchi yanaweza kuwasafishia njia kuelekea ubingwa wa tano mfululizo kwenye ligi.
Hivvyo mchezo huu ni kama fainali, Wananchi wakihitaji matokeo ya aina moja tu, USHINDI.
Leo asubuhi Yanga imeendelea na maandalizi yake visiwani Zanzibar kabla ya kuanza safari ya kurejea Bara.





