Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema maandalizi kuelekea mchezo wa fainali kombe la Muungano dhidi ya Simba yanaendelea vyema na wamejipanga kushinda mchezo huo.
Walter amesema mchezo huo ni wa kipekee kwani unazikutanisha timu mbili zenye ushindani wa asili lakini upande wao kama mabingwa watetezi, wamejipanga kutetea taji hilo.
"Sisi tuko hapa Zanzibar tukiwa na lengo moja tu, kutetea ubingwa wa kombe la Muungano. Mipango yetu ilikuwa wazi tangu mwanzo"
"Tulikuwa tayari kupambana na yeyote atakayekuja mbele yetu na kwa bahati nzuri fainali imekuwa dabi ya Kariakoo"
"Itakuwa fainali ya kipekee ambayo itazikutanisha timu mbili zenye historia ya kipekee, sisi tuko tayari na tunawaahidi mashabiki wetu tunakwenda kupambana ili kutetea ubingwa," alisema Walter
Yanga itakamilisha maandalizi yake ya mwisho leo kuelekea mtanange huo utakaopigwa Jumatano, saa 2:15 usiku