Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake kitaingia dimba la KMC Complex hapo kesho kusaka ushindi kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora kombe la CRDB dhidi ya TMA Stars.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Goncalves amesema anatambua mchezo huo sio wa kuhesabu pointi bali unahitajika ushindi ili kusonga mbele.
Kocha huyo raia wa Ureno amesema anafahamu kwa TMA utakuwa mchezo wa kipekee kwao na anafahamu timu za madaraja ya chini hucheza kwa nidhamu kubwa zinapokutana na timu kubwa ikiwa pia ni nafasi kwa wachezaji wao kuonekana.
Amesema wanapaswa kuchukua tahadhari zote na kuzingatia mpango wao wa mchezo huo ili kupata ushindi na kutinga robo fainali.
“Tunaelekea kwenye mashindano yenye hadhi ya kipekee. Kesho hatuendi kutafuta alama bali ushindi. Wapinzani wetu wanafahamu vyema kwamba mpira wa miguu una maajabu yake. Nakumbuka mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Cosmopolitans ulikuwa mgumu sana. Nilichogundua ni kwamba timu za madaraja ya chini hucheza kwa nidhamu sawa na zile za ligi kuu. Ni lazima tucheze kwa umakini na tahadhari.”
“Ni lazima tucheze kwa bidii na umakini, bila kujali kama tunakutana na Al Ahly au TMA. Tusipokuwa waangalifu tutajikuta tumejiingiza kwenye hali ngumu kwani wapinzani wetu hawana cha kupoteza. Sisi tukipoteza kesho, tutakuwa tumepoteza ubingwa. Iwapo tutatekeleza kila jambo ipasavyo tuna nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa tena.”
“Najua vijana wengi wa TMA wanafahamu kuwa kesho ni jukwaa muhimu la kuonesha uwezo wao. Lazima tuzingatie hilo, lakini hatupaswi kupoteza malengo yetu. Tunajua wameitoa timu ya ligi kuu, kwahiyo sio timu ya kuibeza. Niwaombe sana mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupatia hamasa,” alisema Goncalves