Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanja wa KMC Complex kesho Jumamosi, April 11 kuipa hamasa timu yao katika mchezo wa kombe la CRDB dhidi ya TMA Stars.
Kamwe amesema wanahitaji kushinda mchezo huo ili kutinga robo fainali na kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo kwenye michuano ya kombe la CRDB kwa miaka mitano sasa.
"Tuna miaka mitano sasa hatujapoteza mchezo kwenye kombe la Shirikisho la CRDB. Ninaamini rekodi hii inakwenda kutuongezea nguvu ya kupambana katika mchezo dhidi ya TMA Stars"
"Muda wa mechi ni saa 12:30 jioni na itapigwa palepale kwenye uwanja wa KMC Complex. Uwanja ambao muda si mrefu utakuwa mali yetu baada ya wenye uwanja kuelekea kusikojulikana(KMC wanaweza kushuka daraja)."
"Kwa Mwanachama na Shabiki wa Yanga huna sababu ya kukosa uwanja wa KMC Complex kesho kwani mchezo unapigwa katika muda mzuri"
"Njoo wewe, rafiki yako na familia yako mje mpate burudani. Hii sio mechi ya kawaida kwa sababu ni hatua ya 16 bora, tumeona kombe la CRDB limetoa matokeo yasiyotarajiwa kwenye baadhi ya mechi," alisema Kamwe.