Mlinda lango wa Yanga Aboutwalib Mshery amewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa kikosi chao kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa kesho Jumamosi, April 04 katika uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake kuelekea mchezo huo, Mshery amesema wamekuwa na nyakati nzuri za kujiandaa na mchezo huo chini ya usimamizi wa makocha wao hivyo wako tayari kuwapa mashabiki wao burudani hapo kesho.
Mshery ambaye kesho anatarajiwa kusimama langoni akichukua nafasi ya Djigui Diarra anayetumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu, amesema yeye na golikipa mwenzake (Hussein Masalanga) wote wako tayari yeyota atakayepewa nafasi atapaswa kuipambania Yanga kwenye mchezo huo.
“Wachezaji wote wa Yanga wapo hapa kwa sababu ya kuipambania timu, Kipa yeyote ambaye atapata nafasi anapaswa kufanya vizuri katika mchezo huo, kwa sasa ligi yetu imekuwa bora sana. Timu nyingi zimeimarika. Waalimu wamefanya tathmini sahihi ya michezo iliyopita na kufanyia kazi.”
“Walimu wetu wamefanya kazi nzuri kwenye uwanja wa mazoezi, mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutakuwa na soka safi."
"Tunawahakikishia wananchi kwenda kupambana kwa ajili ya furaha yao. Tunafahamu michezo kadhaa iliyopita haikwenda kama tulivyotarajia. Ni muda sasa wa kuwapa burudani wananchi na kusahau yaliyopita,” alisema Mshery