Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga wako mkoani Singida kuwakabili walima alizeti wa Singida Black Stars. Ni katika mechi itakayopigwa saa 10 jioni katika uwanja wa Airtel.
Ni mechi inayotarajiwa kuwa na upinzali mkali kila timu ikishuka uwanjani kuwania alama tatu muhimu.
Baada ya kudondosha alama mbili kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba, vijana wa kocha Pedro Goncalves leo watashuka uwanjani wakiwa na dhamira moja tu, kuondoka na alama zote tatu.
Singida wametoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo uliopita ambao ulipigwa katika uwanja huo. Hivyo leo watahitaji kuendeleza wimbi la ushindi ukiwa ni mchezo wa pili kupigwa kwenye dimba hilo.
Yanga ilitua Singida juzi ambapo jana kikosi kilipata nafasi ya kujifua dimba la Airtel, nyota wote waliosafiri na timu wakiwa tayari kwa mchezo huo.
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kukosa mchezo huo kutokana na changamoto za majeruhi ni beki wa kati Dickson Job ambaye alipata majeraha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba.
Wachezaji wengine ni Pacome Zouzoua ambaye bado hayuko 'fit' kwa asilimia 100 na Edmund John anaendelea kuuguza maumivu ya bega.