Mechi tano zinazofuata za ligi kuu zinakwenda kuwaweka kwenye majaribu mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga katika mkakati wao wa kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.
Mechi zote Wananchi watakuwa ugenini na zinachezwa kwa wastani kila baada ya siku tatu. Ama kwa hakika ni ratiba ngumu ambayo itawahitaji wachezaji wote kuwa kwenye utimamu wa mwili na saikolojia.
Jana Yanga imetua Singida kuwakabili Singida BS ikitokea Zanzibar kuwakabili watani zao Simba katika mchezo uliomalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Yanga haikupata ahueni na italazimika kucheza mechi nyingine ngumu hapo kesho March 05 wakati watani zao Simba watashuka dimbani March 07 kucheza mechi ya kombe la CRDB.
Baada ya mchezo dhidi ya Singida BS, Wananchi watalazimika kurudi Dar haraka kwa ajili ya mchezo wa kombe la CRDB dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa March 08.
Wakitoka Dar Wananchi watasafiri mkoani Mbeya ambapo March 12 wanapaswa kushuka dimba la Sokoine kuikabili Tanzania Prisons.
Wananchi wakimalizana na Prisons wanapaswa kurudi Dar haraka kwa ajili ya mchezo dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa March 15 uwanja wa Azam Complex.
Baada ya mchezo dhidi ya Azam Fc, safari huenda ikawa ni Tabora/Arusha kuwakabili TRA United katika mchezo utakaopigwa March 18.
Wakishamalizana na TRA United, Wananchi wanapaswa kuelekea Dodoma haraka kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa March 21 dimba la Jamhuri.
Ni ratiba ngumu ambayo ni wazi kocha Pedro Goncalves atahitaji huduma ya kila mchezaji kikosini ili kuvuka salama.