Ilikuwa miezi, wiki, siku na sasa zimebaki saa chache kuelekea mchezo wa ligi kuu unaozikutanisha timu zenye upinzani wa jadi, Yanga na Simba.
Ni katika uwanja wa New Amaan Complex, Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye mchezo unaotarajiwa kuanza majira ya saa 2:15 usiku.
Huu utakuwa mchezo wa pili kuzikutanisha Yanga na Simba msimu huu baada ya kukutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambao Yanga waiibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0.
Wakati huu timu hizo zinakutana zikiwa na malengo tofauti. Yanga inazihitaji alama tatu ili kuendelea kujiimarisha kileleni na kuongeza gap la pointi kati yake ya watani zao hao Simba kufikia alama nane.
Endapo Yanga itashinda leo itafikisha alama 31 na kuwaacha watani zao Simba walio kwenye nafasi ya tatu na alama zao 23. Ni wazi matokeo ya ushindi mapema tu yataiweka Yanga kwenye nafasi nzuri ya kuelekea kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.
Pia Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya kibabe dhidi ya watani zao hao kwani Wananchi wameshinda mechi sita mfululizo zilizokutanisha timu hizo kwenye mashindano yote.
Ushindi utamaanisha Wananchi kuendelea kuwatambia wapinzani wao kwa miezi miwili zaidi kabla ya timu hizo kukutana tena kwenye mchezo wa duru ya pili mwezi May 2026.
Mazingira hayo yanafanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi kwani Simba wanauchukulia mchezo huo kama fainali yao kubwa zaidi msimu huu.
Kupoteza mechi sita mfululizo mbele ya Yanga sio matokeo wanayoyafurahia na wakati huu huenda wakafanya kila wanaloweza ili wasifungwe kwa mara ya saba.
Simba wameimarika zaidi baada ya maboresho waliyofanya kwenye dirisha dogo na pengine leo watashuka dimba la Amaan wakilenga kuondoka na alama zote tatu mbele ya Yanga ambayo inaonekana kuwa na kikosi imara zaidi pia ikiwa kwenye 'form' nzuri.
Yanga watakuwa na faida kubwa kucheza uwanja wa New Amaan Complex kwani msimu huu walitumia uwanja huo kwenye mechi za hatua ya makundi ligi ya mabingwa.
Katika mechi tatu walizocheza kwenye uwanja huo, walishinda mechi mbili dhidi ya AS FAR na JS Kabylie huku wakitoka sare dhidi ya Al Ahly wakifunga jumla ya mabao matano.
Ni wazi matarajio ya mashabiki wa Yanga ni kuona timu yao inaendeleza ubabe dhidi ya Simba kwa kuibuka na ushindi wa saba mfululizo