Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo Fc hapo jana katika mchezo wa ligi kuu ya NBC, kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam leo.
Siku ya Jumatano, Februari 25, Wananchi wanakabiliwa na mchezo mwingine wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa uwanja wa KMC Complex.
Ni mwendo wa bandika, bandua kwa Wananchi wakikamilisha ratiba ya mechi za viporo ambapo mpaka sasa bado kuna mechi 6.
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Namungo Fc jana, mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves alisema ratiba sio rafiki lakini wanahitaji kupambana ili kuhakikisha wanafanya vyema katika kila mchezo malengo yakiwa kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo.
Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Yanga itaelekea visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo dhidi ya watani zao Simba utakaopigwa March 1 uwanja wa New Amaan Complex.