Kikosi cha Yanga, leo Jumatano, saa 1 usiku kitaanza kampeni ya kutetea taji la CRDB kwa msimu wa tano mfululizo pale watakapoikaribisha Cosmopolitan katika mchezo utakaopigwa uwanja wa kMC Complex.
Hii itakuwa mechi ya kwanza tangu mabingwa hao wa Tanzania Bara watupwe nje ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL).
Ni wazi leo Wananchi watakwenda kucheza mechi hiyo wakiwa na dhamira ya kuanza kibabe kampeni ya msimu huu na zaidi kuwapoza mashabiki wao baada ya kushindwa kufuzu robo fainali ya ligi ya mabingwa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema malengo ya klabu hiyo ni kutetea mataji yote ya ndani.
Yanga tayari imerejesha kabatini Ngao ya Jamii, huku ikiwa pia imetwaa kombe la Mapinduzi. Bado taji la Muungano, Ligi Kuu na kombe la CRDB
Kampeni ya kutetea kombe la CRDB inaanza leo pale KMC Complex.