Timu ya JS Kabylie ambao ni wapinzani wa Yanga mchezo wa ligi ya mabingwa, wamethibitisha kuwa watatua nchini siku ya Ijumaa tayari kwa mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi siku ya Jumapili.
Kabylie wanatarajiwa kutua Zanzibar Ijumaa jioni na kukamilisha maandalizi yao siku ya Jumamosi katika uwanja wa New Amaan Complex ambao mtanange huo utapigwa Jumapili.
Wakati Kabylie wakitua Ijumaa, Yanga inaendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo huo ambao wanahitaji ushindi ili kuwa na nafasi ya kutinga robo fainali.
Ni mechi ambayo lazima Wananchi washinde, angalau wafunge mabao mawili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali.
Winga Celestin Ecua ambaye anacheza kwa mkopo Kabylie akitokea klabu ya Yanga, atakuwa sehemu ya wachezaji watakaotua nchini lakini hataweza kucheza mchezo huo kutokana na makubaliano ya kimkataba kati ya Yanga na waajiri wake Kabylie.