Mabingwa wa Tanzania, Young Africans SC (Yanga), leo Jumamosi Januari 31, wanashuka dimbani kwenye mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya vigogo wa soka barani Afrika, Al Ahly ya Misri. Mchezo huo wa raundi ya nne ya Kundi B utapigwa saa 10:00 jioni katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo ni wa muhimu sana kwa Yanga, ambayo inahitaji ushindi wa lazima ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania tiketi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
Matokeo yoyote tofauti na ushindi yataifanya Yanga kuingia kwenye presha kubwa katika michezo miwili iliyosalia ya kundi hilo.
Katika mechi iliyopita ambayo ilipigwa Alexandria, Misri, Al Ahly iliibuka na ushindi wa mabao 2–0, kupitia mabao mawili ya mshambuliaji Trezeguet.
Licha ya kupoteza, Yanga ilionyesha ushindani mkubwa hasa kipindi cha kwanza, ikitengeneza nafasi kadhaa ambazo kama wangezitumia vyema wangebadili hatma ya mchezo huo.
Kuelekea mchezo wa leo, Yanga inafahamu wazi kuwa ushindi nyumbani ni muhimu ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele. Al Ahly, yenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya Afrika, inaingia uwanjani ikiwa na faida ya ushindi wa kwanza na ikilenga angalau kupata sare ili kuendelea kuimarisha nafasi yake kileleni mwa kundi.
Uwanja wa New Amaan Complex unatarajiwa kujaa mashabiki wa Yanga, ambao wanatarajiwa kuwa chachu muhimu kwa Yanga katika mchezo huo.
Ni wazi utakuwa mchezo mgumu lakini kwa Yanga ni ushindi tu ambao utawaweka katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo ya kufuzu robo fainali kwani matokeo tofauti yanaweza kuongeza ugumu katika kuisaka tiketi hiyo