Hatimaye Yanga imetambulisha rasmi usajili wa mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurelio aka DEPU raia wa Angola aliyetua Jangwani akitokea klabu ya Radomiak inayoshiriki ligi daraja la kwanza huko Poland.
Depu amewahi kupita kwenye vilabu vya Petro de Luanda ya Angola, Gil Vicente ya Ureno na Vojvodina ya Serbia. Ameitumikia timu ya Taifa ya Angola ambapo ameifungia magoli 15 kwenye mechi 18 wakati huo ikinolewa na kocha wa sasa wa Yanga Pedro Goncalves.
Depu ametua Yanga akichukua nafasi ya mshambuliaji Andy Boyeli ambaye mkataba wake wa mkopo ulisitishwa na mabingwa hao wa nchi.
Mshambuliaji huyo ni pendekezo la Goncalves aliyehitaji kuongeza nguvu eneo la safu ya ushambuliaji ambalo msimu huu lilianza kwa kusuasua baada ya Clement Mzize kuumia na hivyo kupelekea Prince Dube kuwa mchezaji pekee tegemeo katika eneo hilo.
Depu atajumuishwa katika kikosi cha Yanga kinachoshiriki ligi ya mabingwa na pengine Januari 23 atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Al Ahly nchini Misri.
Karibu Jangwani Depu...!