Mikiki mikiki ya michuano ya Afcon 2025 inaanza kutimua vumbi kesho Jumapili, Disemba 21 kwa wenyeji Morocco kumenyana na Comoros katika mchezo utakaopigwa saa 4 usiku.
Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga watakuwa na uwakilishi katika michuano hiyo ambapo nyota wake sita watapeperusha bendera za Mataifa yao.
Jambo la kufurahisha zaidi kwa Wananchi ni kuwa asilimia kubwa ya wachezaji walioitwa ni tegemeo katika timu zao za Taifa na wana uhakika wa kutumika katika michuano hiyo.
Kuanzia mlinda lango Djigui Diarra ambaye ndiye kipa namba moja wa timu ya Taifa ya Mali, walinzi Mohamed Hussein, Dickson Job na Ibrahim Bacca wao wakiwa na uhakika wa kuitumikia Taifa Stars huku Prince Dube nae akiwa na nafasi yake katika kikosi cha timu ya Taifa ya Zimbabwe.
Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto pia amejumuishwa katika kikosi cha Stars na pengine atakuwa tayari kuwasaidia Bacca na Job kwa kuzingatia mikakati ya kocha Miguel Gamondi ambaye ni kama ameamua kuchukua safu yote ya ulinzi ya Yanga.
Mali itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia siku ya Jumatatu, Disemba 22 wakati mechi ya kwanza ya Stars ni dhidi ya Nigeria Jumanne, Disemba 23.
