Klabu ya Yanga ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch), ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimami wa ligi ya Bodi ya Ligi, adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Katika hatua nyingine, Bodi ya Ligi imezikumbusha klabu zake kuendelea kusisitiza umuhimu wa mchezo wa kiungwana na tabia njema mchezoni kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wake.
Ukumbusho huo unafuatia mfululizo wa matukio ya wachezaji kufanya vitendo visivyo vya kiuanamichezo kwa wachezaji wenzao ikiwemo kupiga.
Pamoja na kuhatarisha usalama wa wachezaji, matukio hayo pia yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa ligi jambo ambalo linaweza kushusha hadhi yake na kwamba licha ya adhabu kali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji husika, bado matukio hayo yameonekana kuendelea viwanjani.